kumbuka kuwasiliana nasi kwa ushauri zaidi 0766865041
Utangulizi
Mojawapo ya maamuzi ya mwanzoni kabisa unayohitaji kufanya kwa ajili ya biashara yako mpya ni kuchagua aina ya muundo wa biashara unaoona unakufaa. Uchaguzi unaofanya ni muhimu kwa kuwa utaathiri uwezo na mamlaka ya biashara yako kufanya au kutofanya jambo fulani. Kuwa na aina na muundo sahihi wa biashara kutakusaidia kukuongoza wakati biashara yako iko kwenye mafanikio au wakati wa taabu.
Muundo sahihi wa biashara ndio utakuongoza nini cha kufanya ikiwa utashtakiwa, na kwa namna gani wewe na biashara yako mtatozwa kodi. Kimsingi ziko namna kuu tatu za kuunda biashara, zimeelezewa hapa chini
Biashara inayoendeshwa na mtu binafsi peke yake
Biashara inayomilikiwa na kuendeshwa kwa Ubia
Kampuni yenye ukomo wa madeni
Biashara inayomilikiwa/ kuendeshwa na mtu mmoja
Biashara inayoendeshwa na mtu binafsi peke yake, au Mfanyabiashara pekee ni aina ya biashara ambayo imeenea sana miongoni mwa wajasiriamali nchini. Hii ni biashara ambayo ni rahisi sana kuanzisha kwani mmiliki hufanya usajili wa jina la biashara na kutimiza masharti mengine machache kabla ya kufungua bishara.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) imetoa mwongozo wa kusajili jina la biashara ambapo mjasiriamali atatakiwa kulipia wastani wa Shilingi 20,000. Mwongozo huu unapatikana kwenye tovuti ya Brela. Mada zijazo pia tutajadili namna ya kusajili biashara.
Biashara inayomilikiwa na mtu mmoja inaweza kuendeshwa kwa jina la mmiliki au jina jingine lisilo lake. Biashara ya aina hii imejipatia umaarufu mkubwa sana kutokana na urahisi wake, haswa katika uanzishaji, pamoja na gharama ndogo. Mfanyabiashara anahitaji tu kujisajili au kusajili jina lake na kupata leseni na hivi hutosha kuanza kufanya biashara.
Hasara kubwa ya kipekee ya muundo huu wa biashara ni kuwa mmiliki anabeba majukumu kwa madeni yote ya biashara yake. Hivyo ikiwa atapata matatizo ya kifedha, wadeni wanaweza kufungua kesi/ madai dhidi yake na yakifanikiwa yeye binafsi atawajibika kulipa madeni hayo kutoka kwenye vyanzo binafsi vya fedha.
Ubia
Hii ni biashara inayotambulika kisheria inayofanywa na watu wawili au zaidi wanaoshiriki katika umiliki, utendaji na faida au hasara za biashara hiyo. Ziko aina kuu mbili za ubia, ubia wa jumla (usio na ukomo wa madeni) na ubia wenye ukomo wa madeni.
Katika ubia usio na ukomo wa madeni (ubia wa jumla), wabia wanaendesha biashara na wanawajibika kwa madeni ya biashara na mali zao binafsi zinaweza kulipia madeni hayo. Kwenye ubia wenye ukomo wa madeni, baadhi ya wabia huwa na ukomo wa kuwajibika kwa madeni ya biashara na baadhi huwa hawana. Wale wasio na ukomo wa kuwajibika kwa madeni ya biashara wanamiliki biashara na wanawajibika binafsi kwa madeni ya biashara, na wale wenye ukomo huwekeza tu, hawana nguvu ya moja kwa moja katika maamuzi ya biashara na hawawajibiki kuchangia fedha binafsi kulipa madeni ya biashara.
Uwajibikaji binafsi wa wabia kwa madeni ya biashara ni suala kubwa la kufikiria iwapo unatazamia kuendesha biashara kwa mfumo wa ubia. Kama ilivyo kwa wafanyabiashara wanaomiliki biashara peke yao, wabia wanawajibika kwa fedha zao binafsi kulipia madeni ya biashara. Kila mbia wa jumla (asiye na ukomo wa madeni) anaweza kufanya maamuzi na kuingia katika makubaliano ambayo wabia wenzake wote watayaheshimu na yatawaathiri (kutegemeana na makubaliano/ mkataba wa ubia wao) kwa niaba ya biashara.
Kumbuka kuwa biashara ya ubia ina gharama kubwa zaidi kuianzisha na kuiendesha kuliko biashara ya mtu binafsi, hii inatokana na ukweli kuwa kuna taratibu mbalimbali inabidi zifuatwe kabla ya biashara kuanza. Taratibu hizo ni pamoja na kuweka makubaliano ya namna ya kuendesha biashara, mgawanyo wa mapato na mengine mengi.
Ikiwa utaamua kuendesha biashara kwa mfumo wa ubia, hakikisha kuwa umeweka kimaandishi makubaliano au mkataba kuonesha namna maamuzi yatakavyofanyika, namna ya kumaIiza tofauti zinazotokea katika kufanya maamuzi, na hata namna ya kufikia makubaliano ya kubadilisha umiliki wa biashara itakapohitajika kufanya hivyo. Makubaliano hayo yanasaidia sana pale itakapotokea kwa sababu moja au nyingine biashara imeingia katika matatizo ya kifedha au ya kiuendeshaji, au ikitokea mbia mmojawapo anataka kuondoka kwenye biashara.
Mkataba wa ubia unapaswa kukazia kuhusu kusudi la biashara na mamlaka na wajibu wa kila mbia. Ni vema kupata msaada wa kisheria kutoka kwa mwanasheria mwenye uzoefu na mambo ya biashara ndogo na za kati katika kuandika mkataba wa ubia. Mambo mengine ambayo ni muhimu yazungumziwe katika makubaliano ya ubia ni:
Umiliki utachangiwa kwa viwango gani? Si lazima viwango vya umiliki na na mgawanyo wa majukumu vilingane kati ya wabia wote. La msingi ni kuhakikisha kiwango cha kila mmoja kiko katika makubaliano.
Maamuzi yatafanyika kwa mtindo gani? Ni vema kuweka makubaliano juu ya haki za kupiga kura baina ya wabia ikiwa wameshindwa kufikia muafaka kwenye suala fulani. Ikiwa wabia ni wawili tu na umiliki wao ni nusu kwa nusu, uko uwezekano wa kushindwa kufikia muafaka katika kuamua jambo. Kuepusha hili, biashara zingine huamua kuweka mbia wa tatu, mtu anayeaminika na kummilikisha asilimia ndogo tu ya biashara, ili kusaidia kuiondoa biashara kwenye mkwamo wa aina hiyo.
Ikiwa mbia mmoja atajiondoa, kiasi cha kumlipa kitaamuliwaje? Namna mojawapo ya kuamua kuhusu hili ni kuwa na mhusika aliye nje ya ubia, mfano benki, au mhasibu kutafuta mtathmini atakayethaminisha kiasi cha kumlipa mbia anayejitoa katika ubia.
Ikiwa mbia atajitoa katika biashara, ni lini anapaswa kulipwa fedha yake? Hii inaweza kuwekwa katika makubaliano ili ijulikane bayana. Ikiwa itachukua muda mrefu, inaweza kuwa busara kuweka makubaliano kuwa ilipwe pamoja na riba. Bila makubaliano haya uendeshaji biashara unaweza kuathirika ikiwa mtu atajitoa na kiasi chote kulazimika kulipwa kwa mkupuo kwa haraka mara anapojitoa. Kampuni yenye ukomo wa madeni
Kampuni yenye ukomo wa madeni ni muundo wa shirika ambamo uwajibikaji wa wamiliki (wanahisa) kwa madeni ya biashara unakomea kwenye kiasi walichowekeza katika kampuni, au ambacho wamekubaliana kukiweka dhamana kwa ajili ya kampuni. Hivyo kampuni yenye ukomo wa madeni inaweza kuwa na ukomo kwa njia ya hisa au ukomo kwa njia ya dhamana waliyoweka wanahisa. Suala la nani anaweza kuwa mwanahisa wa kampuni binafsi linatawaliwa na sheria na kanuni za kampuni.
Kama ilivyo kwa biashara zingine zinazoendeshwa hapa nchini, Kampuni yenye ukomo wa madeni inapaswa kusajiliwa na Mamlaka ya Usajili na Leseni za Biashara, ambayo iko chini ya wizara inayohusika na Biashara. Katika usajili, hatua ya kwanza ni kupata kibali cha kutumia jina la biashara kinachotolewa na mamlaka hiyo. Nyaraka/ taarifa zifuatazo zinahitajika katika mchakato wa kuanzisha kampuni:
Jina la kampuni (ambalo lazima lipitishwe na msajili wa makampuni);
Anuani rasmi ya ofisi ya kampuni Tanzania;
Majina, anuani, na utaifa wa wanahisa wa kwanza na wakurugenzi wa kampuni (angalau wawili kwa kampuni binafsi au saba kwa kampuni ya umma).
Mkataba wa kuanzisha kampuni (unaotaja madhumuni ya kampuni) na sheria/ makubaliano yanayosimamia utendaji na maamuzi ya kampuni (inayotaja muundo wa uongozi na michakato ya maamuzi mbalimbali). Angalau nakala mbili za kila waraka zinapaswa kuwasilishwa.;
Kujaza fomu maalumu zenye tamko kuwa kampuni imezingatia matakwa ya sheria ya makampuni Tanzania; na
Kulipa tozo/ ada za kuwasilisha nyaraka, usajili, na ushuru wa stempu.
Ahsanteni..
kumbuka kuwasiliana nasi kwa ushauri zaidi 0766865041
No comments:
Post a Comment