Tuesday, 24 January 2017

TARATIBU ZA KISHERIA ZA UANZISWAJI WA BIASHARA YOYOTE.



 Kupitia ukurasa huu, napenda kuufahamisha umma, hasa kwa wale wenye njozi ya kuanzisha biashara mpya kwenye ardhi ya Tanzania. Yaweza kuwa mojawapo kati ya biashara zifuatazo, yaani biashara ya mtu binafsi (sole proprietorship), biashara ya Ubia (partnership) na biashara za makampuni.
 
 MMILIKI BINAFSI (SOLE PROPRIETORSHIP) 

Kwa wamiliki binafsi wa biashara wazawa au wageni wanahitaji kuwa na vitu vifuatavyo:
 - TIN - Leseni ya biashara  

.....TIN inatolewa bure na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), hakuna usumbufu katika upatikanaji, inaweza kuchukua siku 1 hadi 2. Jambo la msingi ni kwamba mlipa kodi ni lazima afike ofisi za TRA ili kujiandikisha kupitia biometric scanning inayohusisha kuchukuliwa picha, alama za vidole na sahihi....  

-Akaunti katika benki ya biashara
 
  Kwa mtu ambaye sio raia wa Tanzania anapaswa kuwa na kibali kinachomruhusu kufanya biashara nchini kutoka Idara ya Uhamiaji.      TIN ni kifupisho cha maneno Taxpayer Identification Number, kwa Kiswahili namba ya utambulisho wa mlipa kodi. Ni muhimu kwa mfanyibiashara yeyote kusajiliwa na kutambulika kama mlipa kodi kupitia mamlaka ya mapato Tanzania kwani TIN ni kama uthibitisho wa mfanyabiashara kutambuliwa  na mamlaka na taasisi yoyote ya kibiashara kama vile mamlaka za miji zinazotoa vibali vya biashara pamoja na mamlaka ya mapato yenyewe. Huwezi kufanya biashara na taasisi kubwa kama vile kupewa uzabuni wa kusambaza bidhaa bila kuwa na TIN. Baadhi ya makampuni ya mawasiliano hutoa wakala kwa watu binafsi kutoa huduma za kutuma na kupokea fedha kupitia mitandao ya simu kama vile M-PESA, TIGO PESA, AIR TEL MONEY na mitandao mingine mingi. Moja ya vigezo vikubwa vya kupewa wakala wa mitandoa hii ni kuwa na TIN. Baadhi ya wafanyabiashara wanaochukua uwakala wa kampuni za simu ama kwa kufahamu au kwa kutofahamu wameunganishwa na wakala mwingine katikati na kuwafanya wao kuwa watu wa tatu. Hii inapunguza kamisheni ambayo wakala anapata kwa kuwa kuna sehemu ya malipo inayokwenda kwa huyu mtu wa kati. TIN inatolewa bure na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), hakuna usumbufu katika upatikanaji  wa TIN.

TIN inaweza kupatikana ndani ya siku 1 hadi 2 kutegemeana na idadi ya maombi ambayo mamlaka imepokea kwa kipindi husika.  Mlipa kodi ni lazima afike TRA ili kujiandikisha kupitia biometric scanning inayohusisha kuchukuliwa picha, alama za vidole na sahihi. Katika kukamilisha zoezi hili ni vema muhusika akafika moja kwa moja TRA. Siku hizi kwa ajili ya kugawana ridhiki, wapo watu wa kati wengi ambao husaidia kuwaunganisha waombaji wa TIN na TRA. Watu hawa hutumia ushamba wa watu wengi kujipatia sehemu ya kipato. Si mbaya sana kuwa nao lakini baadhi yao huwatoza wateja wao ujira mkubwa ambao hufanya zoezi la kuomba TIN kuwa na gharama kubwa wakati inaelezwa na mamlaka husika kuwa ni bure. Hata kama muombaji wa TIN atamtumia mtu wa kati ni muhimu yeyemwenyewe kuwepo ili kutoa ushirikiano atakapotakiwa kuchukuliwa picha na sahihi. Lakini pia kufika TRA kwa mfanyabiashara mpya ni muhimu ili kuweza kupata maelezo ya ziada yanahusiana na biashara mpya na msaada wa kitaalamu. Mfanyabiashara atapata fursa ya kuwauliza maafisa wa TRA maswali kadhaa kuhusu biashara kama vile ni kwa nini vipo vyombo vingine vinavyoweza kukamata au kuzuia mzigo unaposafirishwa kutoka duka la jumla, na nini afanye ili kuepukana na usumbufu kama huu? Ni kazi ya maafisa wa TRA kukujibu maswali yote hayo bila malipo kwani ni moja ya kazi walizoajiriwa kuzifanya. Kwa kujisajili kupata namba ya mlipa kodi inaonesha kuwa unatambua wajibu wako kama mfanyabiashara wa kuchangia pato la taifa kwa njia ya kulipa kodi. Na jambo hili ni jema tu kama alivyowahi kusema  Arthur Vanderbilt "Taxes are the lifeblood of government and no taxpayer should be permitted to escape the payment of his just share of the burden of contributing thereto." Na Richard M. Nixonaliyesema “Make sure you pay your taxes; otherwise you can get in a lot of trouble.”

 LESENI YA BIASHARA Unatakiwa kuwa na leseni ya biashara ambayo hupatikana katika ofisi za manispaa husika chini ya Sheria ya Leseni ya Biashara Sura ya 208 kifungu cha 3 ambacho kinasema ni marufuku kufanya biashara bila kuwa na leseni halali katika eneo halali. Muombaji wa leseni anatakiwa kufika katika moja ya ofisi ya afisa biashara katika wilaya au manispaa au mji au katika ofisi za wizara ambao ndio wanahusika na utoaji wa vibali vya biashara katika maeneo husika. Mtu yeyote raia wa Tanzania anayo haki ya kupatiwa leseni ya biashara ili mradi awe ametimiza umri wa miaka kumi na nane (18) mwenye akili timamu ambaye hajawahi kupatikana na kosa la jinai na awe na eneo la kufanyia biashara linalokubalika kisheria. Kwa mtu ambaye sio raia wa Tanzania anapaswa kuwa na kibali kinachomruhusu kufanya biashara nchini kutoka Idara ya Uhamiaji. Baada ya kujaza fomu na viambatanisho, maombi hupitishwa ngazi zinazotakiwa kisheria – Mpango Miji na Afya. Baada ya hapo leseni hutolewa ndani ya siku moja au mbili na si zaidi. Acaunti ya benki itamuwezesha mfanyabiashara kuhifadhi na kupokea fedha kama malipo dhidi ya washirika wake kibiashara.

 2.     BIASHARA YA UBIA (PARTNERSHIP)

 Kwa watu wanaotaka kufanya biashara kwa kuingia ubia ni lazima wafanye kwanza usajili kwa msajili wa makampuni BRELA na kupewa cheti cha umiliki kinachoonesha idadi na majina ya wabia katika biashara husika na asilimia za uchangiaji katika biashara. Katika kuomba TIN wabia watatakiwa kuwasilisha nakala ya cheti cha usajili toka BRELA. Kila mwanachama katika biashara ya ubia atatakiwa kuomba TIN, ikiwa mmoja wao alikuwa nayo hatatakiwa kuomba tena.

 3.     MIFUKO YA DHAMANA

 Mwenye dhamana anatakiwa kuomba usajili BRELA kwanza na kupewa cheti cha usajili kinachoonesha majina na anuani za wenye dhamana . Na pia kila mwanachama anatakiwa kuwa na TIN.

 4.     MASHIRIKA YA UTU

 Taasisi hizi ni lazima zipate ukubali wa kujiendesha kutoka kwa kamishina. Maombi ni vema yakaambatanishwa na nyaraka ambatanishi kutoka wizara ya mambo ya ndani. 5.     KAMPUNI Uanzishaji wa kampuni unahitaji kusajili jina la biashara kwa Wakala wa Usajili wa Biashara (BRERA; Business Regulatory and License Agency). Promota wa kampuni anatakiwa kuwasilisha kwa msajili kanuni za uendeshaji wa kampuni (memorandum and articles of association). Cheti cha ushiriki katika biashara toka BRELA kitaambatanishwa wakati wa kufanya maombi ya TIN pamoja na kanuni za uendeshaji wa biashara. 

UTARATIBU WA KUPATA LESENI YA BIASHARA

  Mwombaji anapaswa kujaza fomu ya maombi 9TFN kikamilifu na kuambatanisha kivuli cha:-
 (i) Jina la Biashara kama sio mtu binafsi (Certificate of Incorporation or Registration).

 (ii) “Memorandum and Article of Association” kama ni Kampuni

(iii) Kitambulisho cha mpiga kura, Cheti cha kuzaliwa au Hati ya kiapo kuonyesha kuwa ni
Mtanzania na Mgeni Hati ya kuishi nchini daraja la “A” (Residnece Permit Class “A”)

 (iv)  Hati ya kiuwakili (prowess of a Honey) kama wenye hisa wote wa Kampuni wapo nje ya nchi.

 (v)  Ushahidi wa maandishi kuwa ana mahali pa, kufanyia biashara (Kwa mfano hati za nyumba, mkataba wa upangishaji, risiti za malipo ya kodi za majengo au ardhi.

 (vi) Hati ya kujiandikisha kama mlipa kodi TRA (TIN). Kwa leseni zinazodhibitiwa na Mamlaka mbalimbali , Kwa mfano (TFDA, EWURA, TAURA, CRB, TILLI) n.k lazima mwomaji kuwa na leseni husika kabla ya kuomba leseni ya biashara. Leseni  hizi hutolewa kulingana na shughuli unayotaka kuifanya, kwa mfano kuna biashara zinalazimisha uwe na leseni kutoka Shirika la Viwango la Taifa (TBS), TFDA, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Baraza la Wakala wa Usalama na Afya mahala pakazi (OSHA) na nyinginezo.

Utaratibu wa wajasiriamali wadogo na wa kati (smes) kuwezeshwa kupata alama ya ubora ya ‘tbs’ Serikali hutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia wajasiriamali wadogo na wa kati pale wanapoomba bidhaa zao wanazozizalisha wenyewe zithibitishwe ubora. Katika utaratibu huu, wapo wajasiriamali ambao husamehewa kulipa ada yoyote kwa sababu ya mitaji yao kuwa midogo. Ili kupata msamaha huu, vigezo vifuatavyo huzingatiwa: Mjasiriamali hutakiwa kuwa na barua ya utambulisho kutoka ofisi ya SIDO iliyo karibu. Ni vema kuhakikisha kuwa barua inafafanua vizuri na kwa kina shughuli zinazofanywa. Kwa wale wanaozalisha vyakula huhitajika kuwa na taarifa fupi kutoka Idara ya Afya iliyo karibu na mahali pa uzalishaji au cheti cha TFDA. Mjasiriamali hupaswa kuwa na leseni ya biashara.  Wajasiriamali waliokwishapata leseni ya kutumia alama ya ubora hupaswa kutunza rekodi za uzalishaji na mauzo ambazo watatakiwa kuzionesha kwa wakaguzi wa TBS pindi zinapohitajika.

HATUA ZA KUPATA ALAMA YA UBORA YA ‘tbs’

1. HATUA YA KWANZA – MAOMBI

Maombi ya uthibitishaji wa ubora wa bidhaa hufanywa na mwombaji kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TBS kwa maandishi. Majibu hutolewa yakielezea taratibu na gharama zote. Majibu huambatana na fomu maalum ambayo mwombaji huijaza na kuirudisha TBS ikiwa na viambatanisho vifuatavyo:  Mtiririko wa uzalishaji wa bidhaa husika;  Mfumo wa uongozi ukionyesha kitengo cha udhibiti ubora; Orodha ya malighafi anazotumia na mahali zinakotoka kwa kila bidhaa; Ramani inayoelekeza jinsi ya kufika kiwandani kwako; Baada ya hapo tarehe ya kufanya ukaguzi wa awali hupangwa.

2.HATUA YA PILI – UKAGUZI WA AWALI

 Ukaguzi wa awali hufanywa na wakaguzi wa TBS wakati kiwanda kikiwa katika uzalishaji. Sampuli huchukuliwa na kupimwa ili kuona kama zinakidhi matakwa ya kiwango husika. Mkaguzi huandaa taarifa kuhusu hali halisi ya kiwanda na mambo yanayostahili kurekebishwa.
.
3 HATUA YA TATU – UPIMAJI Sampuli zilizochukuliwa hupimwa katika maabara za TBS kwa kufuata kiwango husika.  Baada ya kazi ya upimaji kumalizika, ripoti ya maabara hutolewa kwa mwombaji.

4.  HATUA YA NNE – UTOAJI WA LESENI Maamuzi kuhusu kutoa au kutotoa leseni ya kutumia alama ya ubora hutegemea tu ripoti ya ukaguzi wa awali wa kiwanda pamoja na ripoti ya maabara. Kimsingi ripoti zote mbili zinatakiwa kuonyesha kwamba mazingira ya uzalishaji kiwandani, mfumo wa uzalishaji na bidhaa iliyopimwa havina matatizo.  Ikiwa sivyo basi mzalishaji hutakiwa kufanya marekebisho na baadaye mkaguzi wa TBS hutumwa tena na kuleta sampuli nyingine.

MUDA WA LESENI (VALIDITY OF LICENCE) YA ALAMA YA UBORA YA ‘tbs’

Leseni ya kutumia alama ya ubora ya ‘tbs’ hudumu kwa mwaka mmoja na huhuishwa (renewal) baada ya kuhakikisha kwamba taratibu zilizokubalika (Scheme of Inspection and Test, SIT) zinafuatwa.   Biashara za sekta ndogo zinazojihusisha na uvunaji maliasili kama vile uchimbaji madini na madini ya ujenzi (mawe, kokoto, mchanga); uvuvi; kuni na uchomaji mkaa, hazihitaji kusajiliwa na BRELA, bali vibali na leseni zake hutolewa na sekta husika. b. Biashara katika sekta ndogo nyingine zote zinahitaji kusajiliwa na BRELA, yenye ofisi zake jijini Dar es Salaam. c. Kuna kundi la tatu la biashara, ambazo haziko rasmi, na hizi husajiliwa kwa kupewa leseni ya Nguvu Kazi. Leseni za Nguvu Kazi hutolewa na mamlaka za serikali za mitaa chini ya Sheria ya Maendeleo ya Rasilimali Watu, kwa lengo la kuzitambua biashara ndogo ndogo. Idara ya Maendeleo ya Jamii na Idara ya Maendeleo ya Ushirika katika ngazi ya halmashauri zinahusika tu katika kusajili vikundi vya wakulima na wafanyabiashara katika maeneo yao. Kampuni zote sharti zisajiliwe na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) au mamlaka nyingine inayoruhusiwa kisheria.

 LESENI ZA VILEO

 Sheria ya leseni za vileo imenyambulisha aina tisa za leseni za vileo zinazoweza kutolewa chini ya sheria hii: Retailers On Leseni hii humruhusu mwenye biashara kuuza pombe na kunywa eneo la biashara RETAILERS OFF  Leseni hii haimruhusu mtu kinywea pombe eneo la biashara bali kwa watu wanaochukua kunyewea majumbani (Take away) kama Groceries. WHOLESALE Leseni hii ni kuuza pombe kwa jumla HOTEL Leseni hii humruhusu mwenye leseni kuuza pombe kwa ajili ya kunywea katika eneo la biashara kwa watu waliopanga hotelini kwa wakati wowote wa mchana na usiku  RESTAURANT Leseni hii inamruhusu mwenye leseni kuuza pombe kwa mtu yeyote anayekula chakula katika mgahawa katika muda wa saa 6.00 mchana hadi saa 8.00 mchana na saa 12.00 hadi saa 6.00 usiku. MEMBERS CLUB Leseni hii huruhusu uuzaji wa pombe kwa kiasi chochote kwa mwanachama wa Klabu na wageni wao tu COMBINED 4 Leseni ambazo zimeambatanishwa mhili kwa pamoja:

 (a) Combined Hotel and retailers on

 (b) Combined Hotel and Restaurant

 (c) Combined restaurant and retailers on TEMPORARY Leseni hii humruhusu mwenye leseni kuuza pombe katika sehemu iliyotajwa kwenye leseni mahali penye burudani, starehe au mkusanyiko mwingine kwa kipindi kisichozidi siku tatu LOCAL LIQUOR Class A Local Liquor Leseni hii humruhusu mwenye leseni kutengeneza pombe za kienyeji katika sehemu iliyotajwa na kuuza kwa ajili ya kunywea sehemu ya biashara au nje ya sehemu ya biashara Class B Local Liquor Leseni hii humruhusu kutengeneza pombe ya kienyeji sehemu iliyotajwa na kwenda kuuzia sehemu nyingine iliyo na leseni ya kuuza pombe za kienyeji Class C Local Liquor Leseni hii humruhusu kutengeneza pombe ya kienyeji katika sehemu iliyotajwa kwenye leseni na kuuza kwa mwenye class D au Class E Class D Local Liquor Leseni hii humruhusu kuuza pombe za kienyeji katika sehemu iliyotajwa kwenye leseni kwa kunywea eneo la biashara Class E Local Liquor Leseni hii humruhusu kuuza pombe za kienyeji kwa ajili ya kunyewea sehemu nyingine mbali ya eneo la biashara

 MASHARTI YA KUPATA LESENI

 Mtu yeyote raia wa Tanzania anayo haki ya kupatiwa leseni ya Vileo ili mradi awe ametimiza umri wa miaka kumi na nane (18) mwenye akili timamu ambaye hajawahi kupatikana na kosa la jinai na awe na eneo la kufanyia biashara linalokubalika kisheria. Kwa mtu ambaye sio raia wa Tanzania anapaswa kuwa na kibali kinachomruhusu kufanya biashara nchini kutoka Idara ya Uhamiaji.

 UTARATIBU WA KUPATA LESENI

 • Mwombaji hujaza fomu za maombi zinazotolewa na Manispaa
 • Eneo/jingo linalokusudiwa kufanyia biashara hiyo kukaguliwa na Afisa Afya, Afisa Mipangomiji, Polisi, Afisa Mtendaji wa Kata (WDC) na Afisa Biashara wa Manispaa na hutoa maoni yao kwenye fomu husika
 • Maombi hayo hupelekwa katika Malaka ya Utoaji wa Leseni za Vileo ya Manispaa kwa uamuzi
 • Mwombaji ambaye maombi yake yamepitishwa hupewa Leseni baada ya kulipa ada inayotakiwa na ni lazima amekamilisha masharti ya kupata leseni hapo juu MASHARTI YA UTUMIAJI Leseni za vileo zina masharti mengi ikiwa ni pamoja na kutouza kilevi 6 kwa watoto. Masharti mengine ni muda wa kuuza pombe na kelele za muziki. MUDA WA KUUZA POMBE BAA (RETAILERS ON) • Jumatatu hadi Ijumaa - Saa 12.00 jioni hadi saa 5.00 Usiku
 • Jumamosi, Jumapili na Sikukuu - Saa 5.00 asubuhi hadi saa 8.00 mchana na saa 12.00 jioni hadi saa 6.00 usiku GROSARI (RETAILERS OFF)
 • Jumatatu hadi Ijumaa - Saa 2.00 asubuhi hadi saa 1.00 jioni
 • Jumamosi, Jumapili na Sikukuu - Saa 3.00 asubuhi hadi saa 6.00 mchana RESTAURANT LICENCE (MGAHAWA)
 • Jumatatu hadi Ijumaa - Saa 6.00 mchana hadi saa 8.00 mchana na saa 12.00 jioni hasi saa 6.00 usiku
 • Jumamosi, Jumapili na Sikukuu - Saa 5.00 asubuhi hadi saa 8.00 mchana na saa 12.00 jioni hadi saa 6.00 usiku MAKOSA Baadhi ya makosa chini ya sheria hii:
 • Kuruhusu biashara nyingine isiyokubalika kisheria kufanyika eneo la biashara
 • Kuuza pombe kwa mtu mwenye umri chini ya miaka kumi na sita (16)
 • Kuajiri mtu chini ya miaka kumi na sita (16) kuuza pombe
 • Kuruhusu mtu mwenye umri chini ya miaka kumi na sita kukaa eneo la kuuzia pombe
 • Kutoweka leseni sehemu ya wazi, ambapo itaonekana kwa urahisi na wakaguzi
 • Kumruhusu/kuleta fujo katika eneo la biashara
 • Kuruhusu eneo la biashara kutumika kama danguro
 • Kuuza pombe muda ambao ni kinyume cha sheria
 • Kufanya biashara ya pombe kwa kutumia leseni ya vileo ambao haistahili ADHABU Mfanyabiashara anayetenda mojawapo ya makosa haya akikamatwa, atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atalipa faini au kifungo au adhabu zote kwa pamoja.

 UTARATIBU WA USHURU WA MALAZI (HOTEL LEVY) CHINI YA SHERIA NA. 23 YA 1972 MASHARTI YA KULIPIA HOTEL LEVY 

 1. Kila mmiliki wa nyumba ya wageni (Guest House) anapaswa kulipa kodi ya asilimia ishirini (20) ya malipo ya nyumba (Guest House charges) kwa mwezi husika. Wamiliki wenye mauzo yanayotozwa kodi ya zaidi ya Tshs. 40 milioni kwa mwaka hawatalipa kodi ya malazi bali watalipa Kodi ya ongezeko la tghamani (VAT)

 2. Kodi iliyowekwa, italipwa kuanzia tarehe moja hadi tarehe saba ya mwezi unaofuata mauzo

 UTARATIBU WA KULIPIA HOTEL LEVY

 • Malipo ya Ushuru wa Malazi ni lazima yaambatanishwe na fomu ya mapato ya kila siku (fomu H.L. 1) au kitabu cha wageni, na fomu ya mapato ya kila mwezi (fomu H.L.2)
 • Mmiliki wa nyumba analeta fomu H.L.1 au kitabu cha wageni pamoja na fomu H.L. 2 ambaye amekwisha jaza. Afisa anayekadiria atapitia H.L.1 au kitabu cha wageni na fomu H.L. 2 ili kuhakikisha ni sawa na kuhakikisha mmiliki amefikia vizuri asilimia 20 ya mapato ya malazi ya mwezi.
 • Mmiliki akishindwa kulipa ushuru kwa muda uliopangwa, siku saba (7) baada ya mwezi husika kumalizika, atalipa nyongeza ya asilimia 25 ya ushuru unaotakiwa kulipwa, na endapo ataendelea kutokulipa adhabu (penalty) itakuwa inaongezeka kwa asilimia kumi (10) ya ushuru uliotakiwa kulipwa kila baada ya siku thelathini (30) kumalizika

MAKOSA  

 • Mmiliki wa nyumba ya kulala wageni kushindwa kulipa ushuru wa malazi kwa muda unaotakiwa
 • Kushindwa au kukataa kuwasilisha fomu ya mapato ya kila mwezi
 • Kushindwa kuweka na kutunza kitabu chenye kumbukumbu sahihi za kulala wageni
 • Kushindwa kutoa risiti, hati za madai na kumbukumbu nyinginezo kama sheria inavyotaka
 • Kumzuia Mkurugenzi au Mwakilishi wa Mkurugenzi katika kufanya kazi zake zilizowekwa na sheria au Kanuni za Ushuru wa Malazi
 • Kushindwa kutekeleza Ilani iliyotolewa na Kamishna/mkurugenzi ya kuitwa na kuwasilisha nyaraka zinazohusu nyumba yake ya kulala wageni
 • Kutoa taarifa ya uongo kwenye kumbukumbu yeyote inayotumika kwa ajili ya kudanganya au kushindwa au kukataa kujibu maswali vizuri kwa Afisa wa Serikali aliyepewa madaraka na sheria hii

ADHABU 

 • Mmiliki atakayetenda mojawapo ya makosa yaliyotajwa hapo juu atalipa faini isiyopungua Tshs. 50,000.00 kwa Mkruugenzi wa Manispaa na isiyozidi Laki tano (500,000.00) Mahakamani akipatikana na hatia.
 • Mmiliki anayekwepa kulipa Ushuru wa Malazi kwa makusudi akikamatwa na kutiwa hatiani atalipa faini isiyozidi shilingi milioni mbili (2,000,000.00) Hata hivyo kila halmashauri ya wilaya na miji zina utaratibu wake ambao ni vema mfanyabiashara akachukua hatua katika kufahamu ili kuepuka uvunjaji wa kanuni za uendeshaji wa biashara na kuepuka adhabu.

NAWATAKIA MAADALIZI MEMA KATIKA KUFIKIA MALENGO YENU.

KUMBUKA "Usikate tamaa,lakini acha maneno anza vitendo"  

No comments:

Post a Comment