kumbuka kuwasiliana nasi kwa ushauri zaidi 0766865041
1.0 UTANGULIZI
Serikali hutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia wajasiriamali wadogo na wa kati pale wanapoomba bidhaa zao wanazozizalisha wenyewe zithibitishwe ubora. Katika utaratibu huu, wapo wajasiriamali ambao husamehewa kulipa ada yoyote kwa sababu ya mitaji yao kuwa midogo.
Ili kupata msamaha huu, vigezo vifuatavyo huzingatiwa:
Mjasiriamali hutakiwa kuwa na barua ya utambulisho kutoka ofisi ya SIDO iliyo karibu. Ni vema kuhakikisha kuwa barua inafafanua vizuri na kwa kina shughuli zinazofanywa.
Kwa wale wanaozalisha vyakula huhitajika kuwa na taarifa fupi kutoka Idara ya Afya iliyo karibu na mahali pa uzalishaji au cheti cha TFDA.
Mjasiriamali hupaswa kuwa na leseni ya biashara.
Wajasiriamali waliokwishapata leseni ya kutumia alama ya ubora hupaswa kutunza rekodi za uzalishaji na mauzo ambazo watatakiwa kuzionesha kwa wakaguzi wa TBS pindi zinapohitajika.
2.0 HATUA ZA KUPATA ALAMA YA UBORA YA ‘tbs’
2.1 HATUA YA KWANZA – MAOMBI
i) Maombi ya uthibitishaji wa ubora wa bidhaa hufanywa na mwombaji kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TBS kwa maandishi.
ii) Majibu hutolewa yakielezea taratibu na gharama zote.
iii) Majibu huambatana na fomu maalum ambayo mwombaji huijaza na kuirudisha TBS ikiwa na viambatanisho vifuatavyo:
• Mtiririko wauzalishaji wa bidhaa husika;
• Mfumo wa uongozi ukionyesha kitengo cha udhibiti ubora;
• Orodha ya malighafi anazotumia na mahali zinakotoka kwa kila bidhaa;
• Ramani inayoelekeza jinsi ya kufika kiwandani kwako;
Baada ya hapo tarehe ya kufanya ukaguzi wa awali hupangwa.
2.2 HATUA YA PILI – UKAGUZI WA AWALI
• Ukaguzi wa awali hufanywa na wakaguzi wa TBS wa kati kiwanda kikiwa katika uzalishaji.
• Sampuli huchukuliwa na kupimwa ili kuona kama zinakidhi matakwa ya kiwango husika.
• Mkaguzi huandaa taarifa kuhusu hali halisi ya kiwanda na mambo yanayostahili kurekebishwa.
2.3HATUA YA TATU – UPIMAJI
• Sampuli zilizochukuliwa hupimwa katika maabara za TBS kwa kufuata kiwango husika.
• Baada ya kazi ya upimaji kumalizika, ripoti ya maabara hutolewa kwa mwombaji.
2.4 HATUA YA NNE – UTOAJI WA LESENI
• Maamuzi kuhusu kutoa au kutotoa leseni ya kutumia alama ya ubora hutegemea tu ripoti ya ukaguziwa awali wa kiwanda pamoja na ripoti ya maabara.
• Kimsingi ripoti zote mbili zinatakiwa kuonyesha kwamba mazingira ya uzalishaji kiwandani, mfumo wauzalishaji na bidhaa iliyopimwa havina matatizo.
• Ikiwa sivyo basi mzalishaji hutakiwa kufanya marekebisho na baadaye mkaguzi wa TBS hutumwa tena na kuleta sampuli nyingine.
3.0 MUDA WA LESENI (VALIDITY OF LICENCE) YA ALAMA YA UBORA YA ‘tbs’
Leseni ya kutumia alama ya ubora ya ‘tbs’ hudumu kwa mwaka mmoja na huhuishwa (renewal) baada ya kuhakikisha kwamba taratibu zilizokubalika (Scheme of Inspection and Test, SIT) zinafuatwa.
No comments:
Post a Comment